Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Solomon Mndeme ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kwa kuendelea kupata hati safi kwa miaka minne mfululizo.
Mndeme aliyasema hayo kwenye kikao cha baraza la madiwani hivi karibuni kujadili taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali juu ya hoja na mapendekezo ya hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
“Nawapongeza sana Namtumbo hasa kwa waheshimiwa madiwani kwa kuisimamia vyema Halmashauri, viongozi wa wilaya na wataalamu kwa kuonesha ushirikiano na viongozi wa wilaya na kuendelea kupata hati safi kwa miaka minne mfululizo hongereni sana “alisema mkuu wa mkoa huyo.
Pamoja na hayo alipongeza Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kwa kuweza kuchangia kwa asilimia 99.7 mfuko wa wanawake ,vijana na watu wenye ulemavu ambapo kiasi cha shilingi milioni 78 kilichotengwa katika bajeti hiyo kilitumika.
Hata hivyo alimtaka mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Evance Nachimbinya kuwalipa waheshimiwa madiwani stahiki zao kiasi cha shilingi 21,159,000wanazostahili kulipwa kabla ya muda wao kuisha.
Naye mweka hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Pendo Nyomeye alisema Halmashauri hiyo ilikadiria kukusanya shilingi 2,847,746,000 kwa mwaka 2018/2019 na kukusanya kiasi cha shilingi 1,949,514,276 .sawa na asilimia 68.45.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Daniel Nyambo pamoja na kumshukuru mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuipongeza Namtumbo lakini alimshukuru kwa kuitembelea Namtumbo na kutoa maagizo ya kiutendaji na kudai kuwa maagizo hayo ndiyo yanayosababisha utendaji kazi mzuri kwa halmashauri .
Halmashauri ya Namtumbo kwa mwaka wa fedha 2015/2016, 2016/2017, 2017/2018 na 2018/2019 ilipata hati safi.
MWISHO.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: S.L.P 55 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0765142640
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2018Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.