Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo ni moja kati ya Wilaya tano za Mkoa wa Ruvuma uliopo kusini mwa Tanzania, Ambapo Halmashauri ilianzishwa kwa mujibu wa sheria tarehe 02/08/2002 na kupewa kibali rasmi cha uanzishwaji wa Halmashauri Na.366 tarehe 09/11/2006 cha kujitenga kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Songea. Namtumbo ni jina maarufu la Mtemi aliyetoka Msumbiji na kuishi Namtumbo na alikuwa na sifa nzuri kitu kilichomsababishia akawa maarufu. Halmashauri ina eneo la kiutawala lenye ukubwa wa kilometa za mraba 20,375.10 na inachukua 1/3 ya eneo zima la mkoa, Wilaya ya Namtumbo inakadiriwa kuwa na Watu 21 kwa kila kilometa moja ya mraba.
Halmashauri ipo katikati ya Latitudo 9'17' na Latitudo 11'45' kusini mwa mstari wa Ikweta na pia katikati ya Longitudo 35'57' na Longitudo 36'52' kutoka mashariki mwa GMT. Imepakana na Songea upande wa Magharibi, Wilaya ya Ulanga (Mkoa wa Morogoro) kwa upande wa Kaskazini, Wilaya ya Tunduru na Liwale (Mkoa wa Lindi) upande wa Mashariki. Upande wa kusini kuna Mto Ruvuma na mpaka wa kimataifa wa Nchi ya Msumbiji.
Ramani ya Wlaya ya Namtumbo
Wilaya ya Namtumbo ipo kwenye Barabara kuu ya Lami inayounganisha Songea - Tunduru-Masasi-Mtwara/Lindi-Dar Es Salaam ambayo inapitika msimu wote wa mvua na kiangazi na umbali wa kutoka Namtumbo hadi Mji wa Songea ni kilometa 70. Wilaya ya Namtumbo ipo chini mita 200-300 kusini usawa wa Bahari na juu mita 300-500 kaskazini usawa wa Bahari
Hali ya Hewa
Wilaya ya Namtumbo ina hali ya hewa ya wastani wa nyuzi za sentigredi 20-25 kwa mda wa mchana na nyuzi za sentigredi 15-17 kwa mda wa usiku. kipindi cha joto ni miezi ya Septemba, Oktoba, Novemba na Disemba. kipindi cha baridi ni miezi ya Juni, Julai na Agosti. Wilaya ina wastani wa mvua ya mm800 hadi mm1,200 kwa mwaka, huwa mvua inaanza mwishoni mwa Novemba na kumalizika mwezi mei mwaka unaofuata na mvua hupungua nyanda za chini na kuongezeka nyanda za juu. 2/3 ya Eneo lote la Wilaya limezungukwa na Misitu, Miti ya Miyombo, Vichaka, Nyasi na Hifadhi kubwa ya Dunia inayojulikana kwa jina la ''THE SELOUS GAME RESERVE'' ambayo hutoa hifadhi kwa mamilioni ya Wanyama pia eneo ni maalumu kwa kivutio cha Watalii pamoja na ufugaji Nyuki.
Miti ya Miyombo
Wanyama maarufu wa kwenye Hifadhi ya Taifa ya Selous
Eneo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Idadi ya Watu
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 Wilaya ya Namtumbo ina jumla ya takribani watu 201,639 kati ya hao 103,304 au 51% ni wanawake na 98,335 au 49% ni wanaume ikiwa ni ongezeko la ailimia 1.4 kwa mwaka. Kutokana na takwimu za Taifa mwaka 2012, Mamlaka ya Taifa ya Takwimu ilitoa makadirio ya kuwa na watu 225,862 kati yao 110,148 ni wanaume na 115,714 ni wanawake ifikapo mwaka 2017 ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.5 kwa mwaka, ambapo watu wengi wamesambaa kandokando ya barabara kuu ya Songea- Tunduru, Mtwarapachani-Lusewa, Namtumbo-Mgombasi na Mageuzi- Hanga- Kitanda. Nguvu kazi ni kundi la miaka 15-54 ikiwa ni 54% ya watu wote.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: 2 Barabara ya Boma, S.L.P 55, 57382 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0767519181
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.