BARAZA LA MADIWANI NAMTUMBO LARIDHIA JINA LA SEKONDARI YA WASICHANA MKOA WA RUVUMA KUITWA “SAMIA GIRLS SECONDARY SCHOOL”
Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma limepitisha kwa kauli moja kuwa jina la Sekondari ya wasichana ya mkoa wa Ruvuma inayojengwa katika wilaya ya Namtumbo kuitwa SAMIA GIRLS SECONDARY SCHOOL.
Akiwasilisha salamu za serikali katika baraza la madiwani pamoja na mambo mengine mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Dkt Julius Kenneth Ningu alimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 3 za kujenga sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Ruvuma katika wilaya ya Namtumbo.
Dkt Ningu aliwaambia waheshimiwa madiwani kitendo cha ujenzi wa sekondari hiyo inaipa hadhi wilaya ya Namtumbo na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla hali inayotupasa kushukuru kama ilivyoada kushukuru kwa kufanyiwa jambo jema .
Aidha Dkt Ningu aliwaomba waheshimiwa madiwani kuridhia jina la sekondari hiyo kuitwa Samia Girls Secondary School kama shukrani ya wananchi wa Namtumbo kwa Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo za kujenga sekondari ya wasichana wilayani Namtumbo.
Hata hivyo Dkt Ningu aliwaambia waheshimiwa madiwani kilio kikubwa cha wananchi katika wilaya ya Namtumbo ilikuwa bei kubwa ya mbolea lakini wanamshukuru mheshimiwa Raisi kwa kukubali kutoa shilingi bilioni 150 kwa ajili ya kupunguza bei ya mbolea ili kuwapunguzia wakulima bei ya mbolea.
Lakini pia Dkt Ningu aliwaagiza waheshimiwa madiwani kuhakikisha wananchi wanaoishi na silaha katika maeneo yao kuzisalimisha kwa msamaha mwisho tarehe 30 mwezi huu septemba 2022 na baada ya hapo wananchi watakao kamatwa na silaha baada ya tarehe hiyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao alisema mkuu wa wilaya huyo.
Diwani wa viti maalumu Zalia Banda akiongea kwa niaba ya madiwani wenzake walimshukuru Mkuu wa wilaya huyo kwa namna anavyowapa ushirikiano katika maswala ya maendelea katika wilaya hiyo na kudai kuwa madiwani wataendelea kushirikiana naye kwa hali na mali.
Zalia Banda pia aliwasilisha ombi kwa mkuu wa wilaya kupitisha barua iliyoombwa na waheshimiwa madiwani inayowasilishwa katika ofisi ya waziri mkuu kuhusu malalamiko ya wananchi kuhusu kukithiri kwa mifugo katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo na kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara na wafugaji huku waathirika wakubwa ni wakulimwa ambapo Mkuu wa wilaya huyo alikubali kushughulika ombi hilo.
Naye Diwani wa kata ya mkongo Daniel Nyambo kwa upande wake alipendekeza mfumo wa ukusanyaji wa mapato wa Halmashauri utenganishwe kwa madai kuwa mfumo wa ukusanyaji wa kawaida wa mapato hautiliwi maanani na badala yake kutegemea mapato yatokanayo na stakabadhi ghalani.
Nyambo alisema ni vyema mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya kawaida mapato yake yatenganishwe na mapato yanayotokana na ushuru wa papo kwa papo kutoka uuzaji wa mazao kwa njia ya stakabadhi ghalani ili waheshimiwa madiwani wajue badala ya kuunganisha mapato yote.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Jumma Pandu pamoja na kumshukuru mkuu wa wilaya kwa ushirikiano kati ya ofisi yake na waheshimiwa madiwani alisema madiwani wataendelea kuisimamia halmashauri na hawatasita kuchukua hatua kwa watumishi watakaoenda kinyume katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Shule ya sekondari ya wasichana ya mkoa wa Ruvuma iliyopewa jina la Samia Girls Secondary School imejengwa katika kijiji cha Migelegele mamlaka ya mji mdogo wa Namtumbo ambapo Raisi wa Jamhuri wa muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitoa kiasi cha shilingi bilioni 3 ili kujenga majengo hayo.
NA YEREMIAS NGERANGERA
NAMTUMBO.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: 2 Barabara ya Boma, S.L.P 55, 57382 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0767519181
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.