Maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata wamepewa mafunzo kuhusu usimamizi na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana, na walemavu mafunzo hayo yamefanyika leo, Oktoba 04, 2024, katika ukumbi wa Kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo.
Mafunzo hayo yamehusisha maafisa maendeleo ya jamii kutoka kata zote 21 za Wilaya ya Namtumbo yakiwa na lengo la kuimarisha uelewa kuhusu mikakati ya usimamizi wa maendeleo ya jamii, hususani katika kusimamia mikopo ya 10% kwa kufuata taratibu zote zinazotakiwa.
Aidha, mafunzo yameendeshwa na Maafisa maendeleo ya Jamii ngazi ya Wilaya wakiongozwa na ndugu Juma Njelu , ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Namtumbo, ambapo Juma Njelu amesisitiza umuhimu wa mikopo hiyo katika kuboresha maisha ya wanajamii, huku akiwataka maafisa hao kuyazingatia mafunzo ili kuboresha zaidi Utendaji kazi wao katika kusimamia mikopo hiyo.
“Mikopo hii inatoa fursa kwa vikundi vya wanawake, vijana, na walemavu kujiendeleza kiuchumi na hivyo kuchangia katika maendeleo ya jamii nzima, ni matumaini yangu kwamba mafunzo haya wataongeza mara dufu utenda kazi wenu na pia yatasaidia kuleta mabadiliko chanya.” Amesema Njelu
Sambamba na hayo, mafunzo hayo yameletwa wakati ambapo kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha ushirikiano kati ya Halmashauri na vikundi vya maendeleo. Washiriki wamepata nafasi ya kujifunza kuhusu taratibu za kuandika maombi ya mikopo, pamoja na jinsi ya kusimamia fedha hizo kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa, hii inatarajiwa kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali Fedha baina ya Vikundi Husika.
Mbali na hayo, katika kipindi cha mafunzo, washiriki wamehusishwa moja kwa moja katika mijadala, ambapo wameweza kutoa mawazo na maswali kuhusu usimamizi wa mikopo hiyo, pia yametoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kukuza mbinu bora za kazi.
Ikumbukwe, Maafisa maendeleo ya jamii wamehimizwa kuendeleza elimu waliyoipata kwa vikundi vyao ili kuhakikisha rasilimali zinatumika ipasavyo na kusaidia katika kuboresha maisha ya jamii. Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo inaamini kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu ya mabadiliko chanya katika maendeleo ya jamii
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: 2 Barabara ya Boma, S.L.P 55, 57382 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0767519181
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.