VGS ,MTUMISHI WA HALMASHAURI WAKATWA MAPANGA NA WAFUGAJI.
Askari wa wanyamapori wa vijiji (VGS)pamoja na mtumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma wamekatwa mapanga kichwani na wafugaji.
Prisca Msuha Afisa wanyamapori na maliasili wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo alisema mtumishi Issa Ndomondo ambaye Cheo chake ni mhifadhi wanyamapori kutoka katika idara yake ,akiwa na dereva pamoja na askari wa wanyamapori wa vijiji wapatao 8 walitekwa na wafugaji na Kisha kuwacharangwa mapanga.
Prisca alidai mtumishi huyo akiwa na askari wasaidizi wa wanyamapori walitekwa eneo la Nakatete kitongoji Cha milonji mamlaka ya mji mdogo wa Lusewa .
Akisimulia mkasa huo kutoka Hospitali ya Peramiho Kwa njia ya simu Issa Ndomondo Mwenyewe alidai kuwa walitekwa na wafugaji hao wakiwa na mikuki na kuwataka wajisalimishe .
Ndomondo alidai ofisi ilipata taarifa kutoka katika Uongozi wa jumuiya ya Kimbanda kuwa maeneo ya hifadhi yanahalibiwa na wafugaji Kwa kukata miti hovyo na kuendesha shughuli za kilimo na kuchunga mifugo Yao ndani ya hifadhi.
Hata hivyo Ndomondo alisema kuwa walitoa taarifa ofisi ya Mkurugenzi
na kuanza safari ya kwenda kujiridhisha juu ya uharibifu huo lakini wakiwa wanaelekea huko ghafla ndani ya msitu walikutana na kundi la vijana jamii ya wafugaji wenye silaha za jadi na kuwataka wasimamishe na ndipo waliposimamisha na kutakiwa wajisalimishe Kwa kushuka kwenye Hilo gari waliokuwa nalo.
Aidha Ndomondo alifafanua kuwa baada ya kushuka kwenye gari waliwahoji kuwa wanaelekea wapi na ndipo Ndomondo kudai kuwa Jumuiya ya Kimbanda imelalamika kuwa eneo lake limevamiwa na wafugaji hivyo nimetumwa kuja kuangalia uharibifu huo unaofanywa kwenye hifadhi Hali iliyoibua hasira Kwa vijana hao wa jamii za kifugaji.
Kwa Mujibu wa dereva Juma Masuwa baada ya kusimamisha gari na kujionea Hali ya vijana wa jamii ya wafugaji aliamua kutoa gari eneo Hilo na kulirudisha Nyuma walikotoka na akiwa mbali kidogo na kundi lile alishuhudia wenzake wakipigwa mapanga na Kisha wale vijana wa kifugaji kukimbia .
Masuwa aliongeza kuwa alitakiwa na wenzake hao kurudisha gari mpaka eneo la tukio Ili waweze kupanda kuwahi hospitali na wale ambao walikuwa hawawezi walisaidiwa kupanda kwenye gari na kukimbizwa kituo Cha afya Lusewa.
Kaimu Mganga mkuu wa wilaya ya Namtumbo.Dkt. Christopher Wabwarumi alikiri kituo Cha afya Lusewa kuwapokea wagonjwa waliocharangwa mapanga kichwani na kuwapatia huduma ya awali na Kisha wengine kuwapa rufaa ya kwenda Hospitali kubwa Kwa matibabu na uchunguzi zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Chiriku Hamis Chilumba pamoja na kuwataka watumishi kumwombea mtumishi mwenzao aweze kupona alikiri kupokea taarifa hiyo na kuiagiza idara ya wanyamapori na maliasili kuhakikisha watu wote waliopatwa na mkasa huo wanapatiwa matibabu kikamilifu .
Majeruhi waliopatwa na mkasa huo ni Issa Ndomondo mhifadhi wanyamapori, na wengine ni askari wa wanyamapori wa vijiji Twaibu Banda,Kassimu Chai,Rashid Mbelembe,Amina Said,Mwajuma Kalumbi,Omary Komba Ramadhani Musa na Hellena Mbunda ambao Kwa Sasa wamekimbizwa hospitali ya Peramiho Kwa uchunguzi zaidi.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: 2 Barabara ya Boma, S.L.P 55, 57382 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0767519181
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.