WANAFUNZI 3 SHULE YA MTAKATIFU LAURENTI WANUSURIKA KIFO
Wanafunzi 3 wa shule ya mtakatifu Laurenti iliyopo kijiji cha Ruvuma kata ya Hanga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wamenusurika kifo baada ya pikipiki iliyowabeba kugongana uso kwa uso na pikipiki nyingine katikati ya Daraja.
Wanafunzi walionusurika kifo ni France Mustafa Issa(7) wa darasa la kwanza,Fatna Jafari Msuya (8) wa darasa la pili na mwanafunzi Abdurahimu Mustafa Issa (8) wote ni wanafunzi wa shule ya mtakatifu Laurenti .
Kwa mujibu wa mtendaji wa kijiji cha Ruvuma Ziada Mbawala alisema mwendesha pikipiki Hamis Aidini Luambano ambaye ni marehemu alibeba wanafunzi watatu wa shule ya Mtakatifu Laurent akiwapeleka wanafunzi hao shuleni kwa pikipiki yake na alipofika katika daraja la mto hanga waligongana uso kwa uso na dereva mwezake wa pikipiki na kusababisha mwanafunzi Fatna Jafari Msuya atumbukie kwenye mto .
Mbawala alidai Hamisi baada ya kuona mwanafunzi mmoja ametumbukia kwenye mto alijitosa kwenye maji kwenda kumsaka mwanafunzi huyo huku akiwa majini alizidiwa na maji mengi na kuzama ,na mtoto huyo kuokolewa na wasamaria wengine waliofika katika eneo hilo.
Mbawala aliongeza kwa kusema Hamisi Luambano hakuweza kuonekana kwa siku hiyo ya tukio alionekana siku ya pili baada ya maji ya mto Hanga kupungua huku akiwa amepoteza maisha na mwili wake kuzikwa kijiji cha Ruvuma .
Matukio ya kuzama kwa watu na madereva wa pikipiki katika mto Hanga linaongezeka kutokana na daraja la mto huo kuwa jembamba na hapo darajani kuwepo kwa mashimo makubwa hali inayowafanya madereva wa pikipiki wanapofika katikati ya daraja hilo kukutana na mashimo na wanapojaribu kukwepa mashimo hayo huweza kusababisha ajali ya kugongana au kutumbukia ndani ya maji ya mto Hanga.
Daraja hilo lipo kwenye bwana linalozalisha umeme unaotumiwa na watawa wa Abasia ya Hanga ambapo daraja la mto hanga linaonekana kuwa jembamba linalohatarisha watembea kwa miguu ,madereva wa pikipiki na magari wakati wa kupita katika Daraja hilo.
Msababishaji wa ajali hiyo kwa mujibu wa mtendaji wa kijiji cha Ruvuma Ziada Mbawala kuwa ni Peter Ngonyani mkazi wa kijiji cha Hanga na anashikiriwa na jeshi la polisi kwa ajili ya mahojiano na aweze kufikishwa mahakamani .
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: S.L.P 55 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0765142640
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.