ATAMANI NAMTUMBO KUWA NA TIMU LIGI KUU
Mwenyekiti wa chama cha mpira wilayani Namtumbo(NADIFA) mkoani Ruvuma bwana Zuberi Kossa amesema anatamani kuipeleka Namtumbo kupata timu itakayoshiriki ligi kuu Tanzania bara kutoka katika wilaya ya Namtumbo .
Bwana kosa aliyasema hayo katika uwanja wa Taifa katika mamlaka ya mji mdogo wa Namtumbo hivi karibuni wakati akifungua bonanza la michezo mbalimbali iliyowashirikisha watumishi wa kada zote katika halmashauri ya wilaya ya Namtumbo.
Bwana Kossa alidai michezo iliyochezwa wakati wa ufunguzi wa bonanza hilo ni pamoja na mpira wa miguu ,wa pete ,wavu,mchezo wa bao,kufukuza kuku,kuvuta kamba ,kukimbia na magunia,kukimbia na chupa kichwani ,pamoja na kukimbia mbio za mita mia .
Mgeni Rasmi katika bonanza hilo alikuwa katibu tawala wa wilaya ya Namtumbo Aden Nchimbi na katika hotuba yake ya ufunguzi wa bonanza hilo alisema lengo kuu la bonanza hilo ni kumpongeza Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa tena kuiongoza nchi yetu kwa miaka mingine mitano lakini pia kuwaunganisha watumishi wa wilaya ya Namtumbo katika kupata mawazo ya pamoja katika kuiinua michezo wilaya ya Namtumbo.
Afisa michezo wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo bwana John Ligoho alisema pamoja na mambo mengine ipo haja kuziangalia mechi zinazochezwa katika wilaya ya Namtumbo katika timu za wakubwa zinatakiwa kutanguliwa na mechi za watoto waliochini ya miaka 18 ili kuibua wachezaji kutoka katika umri huo .
Ligoho aliongeza kuwa kuwepo kwa mechi za utangulizi zitakazowashirikisha watoto chini ya miaka 18 kutaifanya Namtumbo kuwapata wachezaji wazuri na wenye vipaji na ndio watakaotengeneza timu nzuri ya wilaya ya Namtumbo.
Mwalimu Jeremia Kitwange alisema amefurahishwa sana na bonanza hilo kwani limewafanya watumishi wa idara na vitengo kutoka katika halmashauri ya wilaya ya Namtumbo na wale wa serikali kuu ,Taasisi zisizoza kiserikali na Mashirika ya umma kukutana pamoja , kufahamiana na kucheza pamoja alisema Kitwange.
Mpango wa kuhakikisha wilaya ya Namtumbo inakuwa na timu itakayoshiriki ligi kuu Tanzania bara umeridhiwa na watumishi wote wa wilaya ya Namtumbo katika bonanza hilo na kuweka mikakati ya kuutaka uongozi wa chama cha mpira kuwakutanisha wadau wa mpira na wananchi wote ili kupata michango yao badala ya michango ya upande wa watumishi pekee.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: S.L.P 55 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0765142640
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2018Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.