Baraza la wafanyakazi katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma limepitisha mapendekezo ya mpango na bajeti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kwa mwaka wa fedha unaoanzia julai mosi 2022 na kuishia juni 30,2023.
Akiwasilisha bajeti hiyo kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi , kaimu afisa mipango wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Mohamed Ninje alisema halmashauri hiyo inakisia kukusanya na kupokea jumla ya shilingi 29,824,217,000 kutoka vyanzo vya ndani,ruzuku kutoka serikali kuu na wadau wa maendeleo.
Ninje alidai Halmashauri inakisia kukusanya shilingi 1,984,000,000 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani, ruzuku kutoka serikali kuu shilingi 23,015,526,000 na shilingi 4,131,528,000 kutoka kwa wadau wa maendeleo.
Aidha Ninje pia alifafanua mapendekezo ya matumizi ya bajeti hiyo kuwa shilingi 18,043,444,000 itatumika kwa ajili ya mishahara, huku shilingi 2,663,849,000 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi 9,116,924,000 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Afisa elimu ,elimu maalumu wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Thabiti Mponda aliomba kuongezwa kwa bajeti katika kitengo cha elimu maalumu kwa kuwa mahitaji ya watu wenye mahitaji maalumu yanazidi kuongezeka lakini bajeti imeendelea kumebaki palepale.
Mponda alisikitika kusikia katika bajeti hiyo Halmashauri itajikita katika kuboresha utoaji wa huduma kwa shule mbili maalumu za msingi badala ya shule nne za msingi maalumu zilizopo katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo na kuomba kuongezwa bajeti na kuweka shule nne maalumu badala ya shule mbili .
Mwalimu Rashidi Shaban Mussa (Malimba) alishangazwa na taarifa ya ukusanyaji wa ushuru kituo kikuu cha mabasi cha wilaya ya Namtumbo na kudai kuwa licha ya wadau kushauri katika vikao vikiwemo vya baraza la biashara wilaya ambaye yeye ni mjumbe hakuna jitihada za maksudi za uongozi kuyafanyia kazi mapendekezo ya wadau katika kuongeza ukusanyaji wa mapato katika stendi ya mabasi wilaya ya Namtumbo.
Afisa mipango wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Amos Kanige alisema swala la usimamizi na ufunguzi wa stendi ya wilaya limekamilika hivyo muda wowote kuanzia sasa stendi hiyo itafunguliwa na kuongeza mapato ya Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ambapo magari yatabaki katika stendi rasmi na kupakia abiria hapo tofauti na hivi sasa wasafirishaji abiria hutumia stendi zisizorasmi na kukwepa ulipaji wa ushuru .
Kikao cha baraza la wafanyakazi kupitia mapendekezo ya mpango na bajeti ya Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kilitanguliwa na uchaguzi wa katibu wa baraza la wafanyakazi na katika uchaguzi huo wagombea walikuwa wawili , Shaibu Majiwa Afisa elimu watu wazima na Edigna Muhule afisa mifugo ambapo Shaibu Majiwa aliibuka mshindi kwa kura 27 dhidi ya kura 21 alizopata mshindani wake Edigna Mhule huku wapiga kura walikuwa 50 ikiwa katika upigaji kura hizo 2 ziliharibika.
Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Paul Ambokile pamoja na mambo mengine aliwashukuru wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wilayani Namtumbo kwa kupitia kipengele kwa kipengele na kuridhia kupitisha mapendekezo ya bajeti 2022/2023 na kuhaidi ofisi yake itaongeza ushirikishwaji kwa jamii katika mpango na bajeti ya Halmashauri hiyo ili kuongeza uwazi,ushirikishwaji ,uwajibikaji katika kuleta maboresho katika huduma za jamii.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: S.L.P 55 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0765142640
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.