DC NAMTUMBO AWAKABIDHI WALIMU VISHIKWAMBI 717.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Dkt Julius Kenneth Ningu amewakabidhi walimu wa shule za msingi na sekondari jumla ya vishikwambi 717.
Akizungumza na walimu hao kabla ya kukabidhi vishikwambi hivyo Dkt Ningu alisema serikali ina nia njema ya kutaka kuwaboreshea walimu mazingira ya ufundishaji,ujifunzaji,ufuatiliaji na usimamizi wa elimu kwa kutumia vishikwambi hivyo.
Dkt Ningu alidai kuwepo kwa waratibu elimu kata waliopewa pikipiki na serikali kwa ajili ya kufuatilia maswala ya elimu lakini wakizitumia pikipiki hizo kwa kufanyia kazi zao binafsi za shambani tofauti na malengo ya serikali na kuwataka walimu waliopewa vishikwambi hivyo kutumia kadiri ya malengo ya serikali.
Zoezi la ugawaji wa vishikwambi hivyo liliambatana na utoaji wa taarifa ya matokeo ya kuhitimu darasa la saba ,matokeo ya upimaji darasa la nne na kidato cha pili kwa mwaka 2022.
Afisa elimu shule za msingi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Juma Fulluge katika taarifa yake alidai matokeo ya darasa la saba kwa mwaka 2022 yameshuka kwa asilimia 11ukilinganisha na mwaka 2021 huku waliofanya mitihani ya kuhitimu darasa la saba kwa mwaka 2022 walikuwa 7409 kati ya 7677 waliosajiliwa kufanya mitihani hiyo sawa na asilimia 96.5
Fulluge kwa upande wake pia alitoa taarifa ya upimaji wa matokeo ya darasa la nne na kudai kuwa kwa mwaka huu 2022 ufaulu wa wanafunzi umekuwa wa asilimia 75 .24 na mwaka 2021 asilimia 86.7 huku mwaka 2020 asilimia 97.89.
Hata hivyo afisa elimu sekondari wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Michael Lyambilo katika taarifa yake alisema ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha pili kwa mwaka 2022 umekuwa wa asilimia70.45 ambapo mwaka 2021 ulikuwa asilimia 80.10 na mwaka 2020 ulikuwa asilimia 89.18.
Mkuu wa shule ya sekondari Korido, Oskar Komba alitumia nafasi hiyo kutoa changamoto inayosababisha wanafunzi kufeli ni umbali uliopo kati ya shule na vijiji wanakotoka wanafunzi wanaosoma sekondari kuwa, ni changamoto kubwa kwani wanafunzi hutumia kitambo kirefu kutembea kufika shuleni na wakifika shuleni huwa wamechoka.
Komba aliiomba serikali kuhakikisha jamii inahamasishwa kujenga mabweni ya wasichana na wavulana ili wanafunzi hao wabaki shuleni na kutumia muda wao mwingi katika kujikita na masomo.
Mwalimu Elias Ngonyani wa shule ya msingi Mandela alilalamikia kitendo cha kata,wilaya,na mkoa kutegemea fedha kutoka shuleni ili kuweza kuandaa mitihani mbalimbali ili hali fedha zinazopatikana katika shule hizo hazikidhi mahitaji ya shule na kuomba kata ,wilaya na mkoa iandae mitihani bila kutegemea michango ya fedha kutoka shuleni.
Shule binafsi za sekondari katika matokeo ya kidato cha pili zimeongoza kushika nafasi ya kwanza mpaka nafasi ya tano ,nafasi ya kwanza mpaka ya tatu kwa matokeo ya darasa la nne na nafasi ya kwanza mpaka ya pili kwa darasa la saba 2022.
MWISHO.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: S.L.P 55 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0765142640
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.