DC NAMTUMBO AWATAKA WADAU KUSAIDIA WATOTO WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA HATARISHI.
Aliyasema hayo ofisini kwake wakati wa kumkabidhi mtoto mlemavu (kiziwi)vifaa vya shule ili vimwezeshe kuanza kidato cha kwanza katika shule aliyopangiwa kwenda kusoma.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt Julius Kenneth Ningu alisema mtoto Nasma Yusuph Ismail alifika ofisini kwake kuomba msaada ili akasome kidato cha kwanza katika shule aliyopangiwa, kwa kuwa mzazi wake hana uwezo wa kumsomesha.
Dkt Ningu alidai ofisi yake kwa kushirikiana na ofisi ya mkurugenzi mtendaji wilaya ya Namtumbo kitengo cha ustawi wa jamii walitafuta wadau ili waweze kumsaidia mtoto Nasma aweze kutimiza ndoto yake ya kuendelea na masomo ya sekondari.
Afisa ustawi wa jamii katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Godfrey Mwaulesi alisema shirika la huduma kwa mtoto krasta ya Namtumbo limetoa kiasi cha shilingi 739,900 kwa ajili ya kumwezesha mtoto Nasma fedha na kumnunulia vifaa vya shule.
Mwaulesi alidai kitengo cha ustawi wa jamii katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kinawasiliana kwa karibu na kitengo cha ustawi wa jamii katika Halmashauri ya manispaa ya Iringa kwa ajili ya uangalizi wa karibu wa mtoto huyo akiwa shule ya sekondari ya wasichana ya Iringa .
Mratibu wa shirika la huduma ya mtoto krasta ya Namtumbo alisema shirika liliwiwa na maombi ya mtoto Nasma na kutoa shilingi 739,000 gharama halisi ya mahitaji ya mtoto ili awaze kuhudhuria masomo katika sekondari aliyopangiwa.
Mzazi wa mtoto Ziada Mapunda pamoja na kuishukuru ofisi ya mkuu wa wilaya ,Mkurugenzi alisema bila msaada huo hangeweza kumpeleka shule mtoto huyo kutokana na hali ngumu ya maisha.
Hata hivyo Mapunda alifafanua namna mtoto wake alivyochukuliwa na wasamaria na kumpeleka shule ya viziwi ya mtakatifu vicent ilivyopo manispaa ya songea na kusoma kuanzia darasa la kwanza mpaka kufaulu darasa la saba mwaka 2022 na kupangiwa shule ya wasichana Iringa ambapo bila misaada hiyo alidai hangeweza kumfikisha hapo alipofika na huko anakotaka kwenda.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: 2 Barabara ya Boma, S.L.P 55, 57382 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0767519181
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.