NAMTUMBO WAAJIRIWA WAPYA 146 WAPATIWA MAFUNZO
Waajiriwa wapya 146 kutoka idara ya kilimo,afya ,elimu msingi na sekondari,utawala na maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma walipatiwa mafunzo ya awali kuhusu utumishi wa umma (induction course).
Ofisa Rasilimali watu na utawala wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Hamis Mkele alisema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha waajiriwa wapya waujue mfumo mzima wa uendeshaji wa serikali za mitaa.
Aidha Mkele aliongeza lengo lingine la mafunzo hayo pia lilikuwa kuwajengea uwezo wa namna ya kupata stahiki zao mbalimbali kwa kufuata kanuni,taratibu na sheria za utumishi wa umma zilizowekwa na serikali.
Marietha Chilumba ni mteknolojia maabara hospitali ya wilaya ya Namtumbo pamoja na kuishukuru ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kwa kuandaa mafunzo hayo alidai mafunzo hayo yamemwezesha namna ya kupata stahiki zake za kiutumishi na yamemwezesha namna ya kuingia kwenye mfumo ili aweze kupata barua ya kuthibitishwa kazini pamoja na kujua sheria,kanuni na taratibu za kiutumishi.
Erasto Damiano mwalimu wa Sekondari Namabengo alisema mafunzo waliyoyapata yatawasaidia sana kuzingatia taratibu ,kanuni na sheria za utumishi katika kutekeleza majukumu yao ya kiutumishi lakini pia katika kudai stahiki zao.
Ofisa Teknolojia ya Habari na mawasiliano (TEHAMA) wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Edwin Swai aliwafundisha waajiriwa wapya jinsi ya kuutumia mfumo wa ujifunzaji kielektroniki ili kupata barua ya kuthibitishwa kazini na kutumia mfumo huo kuwasilisha madai yao ya kiutumishi ili waweze kupata stahiki zao.
Mafunzo kwa watumishi wapya yalifanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kwa muda wa siku moja ambapo watumishi wapya kutoka makao makuu ya Halmashauri hiyo pamoja na watumishi wapya waliopo katika kata za Halmashauiri hiyo walihudhuria mafunzo hayo.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: S.L.P 55 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0765142640
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.