WADAU NAMTUMBO WATOA MAAZIMIO MAZITO KUSIMAMIA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI.
Kikao Cha wadau katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma kilichoketi tarehe 18.4.2024 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kilitoa Maazimio mazito katika kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani Wilayani humo.
Awali akisoma taarifa ya uendeshaji mfumo wa stakabadhi ghalani Kwa msimu uliopita wa mwaka 2022/2023 Afisa kilimo,mifugo na uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Paul Ambokile aliwaambia wadau hao kuwa mauzo kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani umewanufaisha wakulima Kwa kiasi kikubwa. Kwa kuuza mazao Yao Kwa bei nzuri na kuwa na uhakika na soko Kwa mazao Yao.
Hata hivyo Ambokile alisema mfumo wa stakabadhi ya ghala ni mfumo unaotumika kisheria chini ya sheria namba 10 ya mwaka 2005 na kutekelezwa Kwa kanuni za mfumo za mwaka 2006.
Issa Issa Ntine mkulima kutoka chama Cha msingi Mliwasi Wilayani humo alisema mfumo wa stakabadhi ghalani ni mzuri Kwa mkulima wa kipato Cha chini lakini akaziomba Taasisi za kibenki kuwasaidia wakulima Kwa kutofunga akaunti zao Kwa kuwa fedha zao ni za msimu ili kuwaondolea usumbufu mara wauzapo mazao Yao kuambiwa akaunti zao zimelala au kufungwa Kwa kutoweka fedha muda mrefu na kuleta usumbufu mkubwa Kwa wakulima hao na wakati mwingine wakulima wanalalamikia kuchelewa kulipwa fedha zao kumbe ni kutokana na Changamoto hizo.
Asedi Kaporo mwenyekiti wa chama Cha msingi Namtumbo pamoja na kusema kuwa mfumo ni mzuri alikiomba chama kikuu SONAMCU kutumia zoni katika kusambaza vifungashio badala ya vyama vya msingi vyote kufuata vifungashio katika eneo Moja ili kurahisisha usafirishaji na upatikani wake Kwa uharaka.
Kaporo alipendekeza zoni za kusambaza vifungashio ziwe nne ambapo alipendekeza zoni ya Lusewa, Namtumbo ,Mgombasi na Hanga ili kurahisisha usambazaji na upatikanaji wa vifungashio Kwa wakulima.
Diwani wa kata ya Mkongo Daniel Nyambo Pamoja na kusema mfumo wa stakabadhi ghalani unawanufaisha wakulima aliwaambia wadau hao kuwa mfumo umeingiliwa na wafanyabiashara ambao hukopesha wakulima fedha ndogo na hulipwa ufuta mwingi na wao kuuza katika mfumo wa stakabadhi ya ghala na kujipatia pesa nyingi.
Nyambo alisikitishwa na kitendo Cha wafanyabiashara katika kata yake ya Mkongo kuwakopesha wakulima fedha shilingi 50,000 na kulipwa ufuta kilo 100 ambapo waliuza katika mfumo wa stakabadhi ghalani na kujipatia 400,000 Kwa bei ya mwanzo Kwa msimu wa 2022/2023.
Nyambo alidai juhudi za maksudi zinahitajika hasa Kwa Taasisi zetu za kibenki kuwakopesha wakulima fedha na pembejeo ili waweze kulima Kwa Tija badala ya kuwa watumwa wa watu wengine.
Diwani wa kata ya Kitanda Charles Chengula alisisitiza suala la ukusanyaji wa mapato, Madiwani ,viongozi wa Serikali kuwa na msimamo wa Pamoja kudhibiti utoroshaji wa mazao na ushuru wa Halmashauri
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya aliwaambia wadau kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani umewawezesha wakulima wa Wilaya ya Namtumbo kupata bei nzuri Kwa mazao ya ufuta,mbaazi na soya Pamoja na kuwa na uhakika wa soko.
Aliwaagiza viongozi wa vyama vya msingi kuhakikisha wanasimamia mfumo Kwa uadilifu mkubwa na kinyume Cha hapo serikali itasimamia haki Kwa wananchi na kuwataka viongozi hao kuondoa dhana kuwa mambo ya ushirika hayaingiliwi .
Hata hivyo Malenya alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Namtumbo kuhakikisha anawaandikia barua watendaji wa kata na vijiji kudhibiti ununuzi holela wa mazao ya wakulima Bila kufuata utaratibu kanuni na sheria zilizopo.
Malenya aliongeza kuwa jitihada za Pamoja za kusimamia ukusanyaji wa mapato na kusimamia kudhibiti utoroshaji wa mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo unahitajika Sana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Philemon Mwita Magesa aliwataka wadau kushirikiana katika kuhakikisha mfumo wa stakabadhi ghalani una wanufaisha wananchi wa Namtumbo.
Magesa alidai kuwepo Kwa wafanyabiashara wanaonunua ufuta Kwa wakulima na wafanyabiashara wanaokopesha fedha Kwa wakulima Kwa fedha ndogo na wakati wa masoko Kwa mfumo wa stakabadhi ghalani unapoanza wafanyabiashara hao hupeleka ufuta na kulipwa fedha nyingi ambazo nazo hazibaki Namtumbo huondoka na kwenda kufanya matumizi maeneo mengine nje ya Namtumbo.
Magesa aliwaambia wadau waliohudhuria kikao hicho kuwa kitendo hicho kina madhara makubwa Kwa maendeleo ya Namtumbo hivyo akawataka wadau kushirikiana Kwa Pamoja kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani Kwa kuwataka wakulima wenyewe wa Namtumbo kuuza mazao Yao Kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ili fedha watakazopata zitabaki Namtumbo Kwa maendeleo ya Namtumbo alisema Magesa.
Viongozi wa vyama vya msingi 47 katika Wilaya ya Namtumbo , viongozi wa vikundi vya wakulima ,wanunuzi wa mazao ,viongozi wa wafanyabiashara ,kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya ya Namtumbo ,wakuu wa idara , Taasisi za kibenki Pamoja na wamiliki wa maghala walihudhuria kikao hicho ..
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: 2 Barabara ya Boma, S.L.P 55, 57382 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0767519181
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.