ZIARA YA DC NAMTUMBO YATAWALIWA NA MALALAMIKO YA WAFUGAJI.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Ngollo Ng’waniduhu Malenya anafanya ziara ya kuzungumza na wananchi wa wilaya ya Namtumbo kwa kusikiliza kero zao na kuzipatia majawabu kero hizo.
Ziara hiyo imeanza leo tarehe 3mei 2023 kwa kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Lingusenguse ,Sasawala,Amani pamoja na kijiji cha Ligunga ambapo kero kubwa kwa wananchi wa vijiji hivyo ilikuwa kero ya wafugaji katika mazingira ambayo wananchi wa vijiji hivyo wanafanya shughuli za kilimo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Sasawala Saidi Mbele alimwomba mkuu wa wilaya kibali cha kuwaondoa wafugaji kwa nguvu ili kuwafanya wananchi wa kijiji chake kufanya shughuli za kilimo bila kuhofia wafugaji kulisha mazao yao .
Mbele alidai wakulima wa kijiji chake wameomba msaada ngazi ya wilaya na mkoa kwa kuomba msaada wa kuwaondoa wafugaji bila mafanikio na kumwomba mkuu wa wilaya huyo kibali cha kutumia wananchi wake kuwaondoa wafugaji hao kwa nguvu.
Omari Yahaya wa kijiji cha Amani wilayani humo alimwambia mkuu wa wilaya huyo kuwa wananchi wanaolima katika maeneo ya hifadhi huondolewa kwa nguvu lakini wafugaji wengi wapo katika hifadhi hizo na hawaondolewi kwa nguvu.
Hata hivyo Yahaya alidai maeneo yaliyotengwa na vijiji kwa ajili ya mapito ya wanyama (ushoroba) kwa sasa maeneo hayo kwa sasa wanyama wametoweka kuwakimbia wafugaji walioenea katika maeneo hayo .
Afisa mifugo wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Paul Ambokile aliwaambia wananchi hao utaratibu wa kuufuata katika kuwapokea wageni katika maeneo ya vijiji vyao lakini akawahatarisha viongozi wa vijiji kuheshimu msimamo na maamuzi ya wilaya kuwa hakuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji katika wilaya ya Namtumbo.
Afisa maliasili na usafi wa mazingira Priska Msuha alikiri kuwepo kwa wafugaji wengi katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya mapito ya wanyama (ushoroba) na maeneo ya misitu na kufanya wanyama wakimbie maeneo hayo .
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo pamoja na mambo mengine aliwahimiza viongozi wa vijiji kuwa wenye mamlaka ya kulinda ardhi ya kijiji ni kijiji chenyewe na kutofanya hivyo kutafanya wafugaji waendelee kuharibu mazingira ya vijiji na kutengeneza migogoro
Ngollo aliwaambia wananchi hao kuwa wafugaji hawajawahi kuwa watunzaji wa mazingira bali wao wamekuwa waharibifu wakubwa wa mazingira na kuwataka viongozi wa vijiji kujua kuwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji ni wilaya ya Tunduru na sio katika wilaya ya Namtumbo.
Hata hivyo mkuu wa wilaya huyo alisema utaratibu wa kuwaondoa wafugaji hao katika maeneo yasiyorasmi unaendelea na kuwataka viongozi wa vijiji kushirikiana na ofisi yake katika kufanikisha jambo hilo.
Ziara ya mkuu wa wilaya huyo kutembelea vijiji vya wilaya ya Namtumbo imeanza leo tarehe 3mei na itamalizika tarehe 8 mei mwaka huu 2023 kwa kuzungumza na wananchi wa vijiji 66 na mamlaka ya miji midogo miwili ya Lusewa na Namtumbo.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: S.L.P 55 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0765142640
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.