Familia sita katika kijiji cha Namanguli kata ya Luchili wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma zimepata pigo la kuezuliwa nyumba zao na upepo mkali ulioambatana na mvua kali na kuziacha familia hizo zikihangaika kwa kukosa makadhi.
Tukio hilo limetokea hivi karibuni, muda wa jioni ambapo mvua iliyoambatana na upepo mkali iliezua nyumba tano za familia moja na moja kutoka katika familia nyingine karibu kabisa na familia hizo tano katika kijiji cha Namanguli wilayani humo.
Walioezuliwa na upepo huo ni pamoja na Shabani Issa, Achumi Issa,Zuberi Issa, Mkwawa Issa ,Saidi Issa pamoja na Osmundi Menas wote wa kijiji cha Namanguli kata ya luchili wilaya ya Namtumbo mkoa wa Ruvuma.
Kaimu mtendaji wa kijiji cha Namanguli bi. Hija Siwea amedai katika tukio hilo hakuna watu walioathirika kwani wakati matukio hayo ya kuezuliwa nyumba hizo yanatokea familia za nyumba hizo zilikuwa bado hazijarudi kutoka shambani.
Bi. Siwea alisema uongozi wa kijiji kwa kushirikiana na mheshimiwa diwani wa kata ya luchili bwana Othmani Njovu waliwatembelea wananchi waliopatiwa na tatizo hilo kwa lengo la kutoa pole kwa waathirika .
Upepo huo pia uliezua shule ya msingi kilangalanga kata ya Luchili jumla ya madarasa 2,shule ya msingi Ligunga mamlaka ya mji mdogo wa Lusewa darasa moja pamoja na shule ya msingi msisima darasa moja katika mamlaka hiyo hiyo ya lusewa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo bwana Evance Nachimbinya alitembelea shule zilizopatwa na majanga hayo na kuchukua hatua ya kuezeka majengo yote yaliyoezuliwa na upepo huo na kuhakikisha shule zote zinaendelea na masomo kama kawaida .
Mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma zimekuwa za upepo mkali zinazoambatana na radi mara kwa mara lakini mvua hiyo imekuwa tegemeo kubwa kwa wakulima wa wilaya ya Namtumbo kwani wanadai mvua ya mwaka huu ni ya kupata mazao mengi kwani inanyesha kwa vipindi hali inayofanya mazao yapate nafasi ya kukua.
MWISHO
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: S.L.P 55 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0765142640
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2018Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.