DC AWASIMAMISHA KAZI WATUMISHI WATATU NAMTUMBO.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Dkt Julius Kenneth Ningu amewasimamisha kazi wakuu wa idara 3 wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kwa muda wa wiki mbili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili katika idara zao wanazoziongoza.
Akiongea kwenye kikao alichokiitisha yeye kwenye ukumbi wa ofisi yake ,mkuu wa wilaya huyo alisema kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Namtumbo imeamua kuwasimamisha kazi wakuu wa idara 3 kupisha uchunguzi unaowakabili.
Aliwataja aliowasimamisha kazi kuwa ni mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii Peres Kamugisha, Lucia Kafumu mkuu wa idara ya afya ,na mwingine ni Samson Manjale mkuu wa kitengo cha Manunuzi katika Halmashauri hiyo.
Dkt Ningu alifafanua sababu ya kumsimamisha kazi Afisa maendeleo ya jamii bwana Peres Kamugisha kuwa ni kuingilia kati manunuzi ya vifaa,mashine katika vikundi vya vijana ,wanawake na watu wenye ulemavu ambavyo vinapewa fedha asilimia 10 kutoka katika Halmashauri .Alidai yapo maelekezo kutoka katika vikundi yanayomtaja afisa huyo kutoa maelekezo ya kununua vifaa au mashine kwa watu wenye bei kubwa tofauti na bei ya soko.
Alitaja sababu ya kumsimamisha mganga mkuu wa wilaya hiyo Lucia Kafumu kuwa ni kushindwa kusimamia ujenzi wa vyoo pamoja na ujenzi wa vyumba vya kujifungulia ambayo fedha yake ililetwa mwezi machi 2021 mpaka sasa ujenzi wake unasuasua licha ya ofisi ya mkuu wa wilaya huyo kulifuatilia jambo hilo kwa muda mrefu bila mafanikio na agizo la kumtaka watumishi wa idara yake kuacha lugha chafu wakati wa kuwahudumia wagonjwa nalo likaonekana pia kushindwa kulifanyia kazi na wananchi wanaendelea kushuhudia lugha chafu alibainisha mkuu wa wilaya huyo.
Hata hivyo mkuu wa wilaya huyo alidai tatizo lingine la mkuu wa idara ya afya ni kutotekeleza maagizo yaliyotolewa na kamati ya ulinzi na usalama ya kumtaka kumchukulia Hatua mtumishi wake mmoja aliyebainika kulewa wakati wa kazi baada ya kamati ya ulinzi na usalama kumtaka kufanya hivyo bila mafanikio.
Mwingine ni Samson Manjali mkuu wa kitengo cha Manunuzi amesimamishwa kwa sababu ya kuingilia taratibu za manunuzi kwa kuzitaka kamati kwenda kununua vifaa kwa baadhi ya wazabuni hali iliyotoa mazingira ya wasiwasi lakini pia upotevu wa mifuko 600 ya smenti ambayo Halmashari ilinunua,upotevu wa boksi 275 za marumaru na Halmashauri kuagiza ununuzi wa mirunda 800 ambayo haieleweki ipo wapi alisema mkuu wa wilaya huyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Jumma Pandu kwa upande wake alisema hapingani na kamati ya ulinzi na usalama kwa mapungufu waliyoyabaini .Hivyo aliomba kamati hiyo ya uchunguzi ifanye kazi ili haki itendeke pasiwepo na mtumishi ambaye ataonewa katika hilo.
KIkao cha kuwasimamisha kazi watumishi hao kimefanyika leo tarehe 28 mwezi aprili katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo ambapo wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo walihudhuria kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Namtumbo pamoja na katibu wa Mbunge wa Jimbo la Namtumbo.
Mwisho.
NA YEREMIAS NGERANGERA
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: S.L.P 55 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0765142640
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.