MABOMU YARINDIMA UGOMVI WA WAFUGAJI NA WAKULIMA NAMTUMBO
Ugomvi wa wafugaji na wakulima katika kijiji cha Amani kata ya Magazini wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma uliibuka mara baada ya wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba ya korosho na kuharibu korosho kwenye mashamba ya wakulima.
Mwenyekiti wa kijiji cha Amani Ismaili Banda alisema kijiji chake hakijapokea wafugaji na hakina eneo la kuwaweka wafugaji lakini wafugaji hao hutoka katika vijiji vingine na kuingia kijiji hicho kuchunga mifugo yao na kulisha mazao ya wakulima.
Banda alisema chanzo cha kurindima kwa mabomu katika mgogoro huo ni wananchi kutoridhika na jeshi la polisi linapopelekewa malalamiko na wafugaji huegemea upande wa wafugaji na kutaka kuwanyanyasa wakulima yaani wananchi wa kijiji cha Amani alisema mwenyekiti.
Mwenyekiti Banda alifafanua kuwa wakulima wawili wa kijiji hicho Mohamedi Mohamedi na mwenzake Obedi Ambali walitoa taarifa kijiji kuwa Ng’ombe wamevamia mashamba yao na kwenda kukamata zile ng”ombe na kuziweka chini ya kijiji kwa hatua Zaidi.
Baada ya Ng”ombe hao kukamatwa mwenyekiti alidai kupigiwa simu na mfugaji aliyejitambulisha kwa jina moja la Nyerere akidai ng”ombe wake wamekamatwa katika kijiji changu na nikamwambia ni kweli aje ofisini kwa ajili ya kuzungumzia swala lake lakini badala yake alipiga simu kwa kamanda wa polisi mkoa na kamanda wa polisi wilaya ya Namtumbo na kisha kuja na polisi kijijini hapo alisema mwenyekiti huyo.
Hata hivyo Banda alisema mara baada ya polisi kufika kijijini hapo walifika kwenye mashamba ya wakulima na kuwatisha wakulima waliokuwa wameharibiwa na mashamba yao ya korosho kwa kusema wameharibu wenyewe na kudai wafugaji wamepitisha mifugo hali iliyowakasirisha wakulima hao alisema mwenyekiti wa kijiji hicho.
Pamoja na ukaguzi huo wafugaji waliwaambia polisi kuwa Ng”ombe wao amechinjwa wakimtuhumu Musa Jongo ambapo polisi walifika nyumbani kwa issa Jongo na kuikuta Ngozi ya Ng”ombe aliyechinjwa hivi karibuni na kutaka kumkamata hali wananchi hao wakijua kuwa bwana Jongo Ng’ombe huyo alinunua kwa ajili ya sikukuu ya Eid el haj.
Kwa mujibu wa Musa Jongo mwenyewe alisema pamoja na kuwaambia polisi hao ng”ombe niliyechinja alinunua kwa ajili ya sikukuu ya Eid el haj hawakutaka kumwelewa na kutaka kumkamata hali iliyoibua hasira kwa wananchi na kudai kuwa hachukuliwi mtu hapo na wananchi wakazidi kupeana taarifa na kuzidi kuongezeka eneo la tukio na ndipo polisi walipojaribu kuwatawanya kwa mabomu wananchi hao wakipiga kelele hatoki mtu hapo na ndipo aliposalimika alisema Jongo.
Issa Yahya mwananchi wa kijiji cha Amani aliwalalamikia jeshi la polisi kwa kuwapendelea wafugaji akidai kijiji hicho kimejifunza kutokana na matendo ya polisi kuwakamata wananchi waliopigana na wafugaji baada ya wafugaji kuingiza mifugo yao katika mashamba yao lakini wafugaji wakaonekana wanabebwa na polisi na wananchi walikaa mahabusu na kijiji kwenda kuwapambania ili waweze kutoka.
Yahya aliongeza kuwa kijiji cha Amani kwa sasa polisi hatuwaamini katika kushughulikia maswala ya migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kuwa wanaegemea upande wa wafugaji na kuwanyanyasa wakulima alisema Yahya .
Mtendaji wa kijiji cha Amani Constantine Gilbat alisema mgogoro huo ulilipotiwa ofisi ya mkuu wa wilaya na mkuu wa wilaya ya Namtumbo kufika katika kijiji hicho kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara na kuweza kurudisha hali ya chuki na kuwa ya Amani tena.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya alizungumza na wananchi wa kijiji hicho huku akiwataka wafugaji kuondoka katika kijiji hicho na kulipa gharama za uharibifu tsh 300,000 kutoka kwa wenye mashamba walizotaka walipwe ili mgogoro huo uishe.
Wananchi wa kijiji cha Amani kata ya Magazini kupitia mikutano yao ya hadhara walikubaliana kutowapokea wafugaji katika kijiji hicho na wafugaji watakaoonekana katika kijiji hicho watakamatwa na serikali ya kijiji hicho na kushughulikiwa kwa mujibu ya sheria na kiongozi yoyote atakayejihusisha na kuwapokea wafugaji katika kijiji hicho ataondolewa madarakani pamoja na kufikishwa mahakamani.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: 2 Barabara ya Boma, S.L.P 55, 57382 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0767519181
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.