MADIWANI NAMTUMBO KUWASILISHA MAPENDEKEZAO KUFUTA HIFADHI
Wakiongea kwenye vikao vya kamati na kikao kazi madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo walipendekeza kufutwa Kwa hifadhi za jamii za vijiji katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo.
Mwenyekiti wa kamati ya uchumi ,ujenzi na Mazingira Charles Chengula alisema malalamiko ya waheshimiwa madiwani ,wananchi wa wilaya ya Namtumbo kuhusu kutenga maeneo ya hifadhi za jumuiya ya Mbarang'andu,Kimbanda na kisungule yalikuwa mazuri Kwa wananchi wa jumuiya hizo lakini Jumuiya hizo zimevamiwa na wafugaji na kuharibu Mazingira ya uhifadhi huo.
Chengula alidai wakulima waliokuwa wanalima katika maeneo ya hifadhi waliondolewa Kwa nguvu na wengine kufikishwa mahakamani na kufungwa Kwa Mujibu wa Sheria lakini wafugaji wapo katika maeneo hayo hayo na kuendesha shughuli zao za kilimo kufuga na kuchunga katika maeneo ambayo wakulima waliondolewa Kupisha uhifadhi.
Hata hivyo Chengula pamoja na mambo mengine alisema malalamiko ya kuwaondoa wakulima katika maeneo ya hifadhi Kwa nguvu huku wafugaji wakiendesha shughuli zao katika maeneo hayo hayo yanawapa wakati mgumu waheshimiwa madiwani kujibu maswali hayo kutoka Kwa wananchi.
Mheshimiwa Chengula aliwataka wajumbe kufikia uamuzi juu ya tatizo Hilo Kwa kuwa Halmashauri kupitia ofisi ya Mkurugenzi wamelalamikia Sana swala la wafugaji kufanya shughuli zao katika maeneo ya hifadhi lakini wafugaji hao wanaishi huko Kwa nguvu na wataalamu wa Halmashauri wanapotaka kufanya kazi ya kuwahamisha wafugaji huwapiga wataalamu hao Kwa kuwajeruhi na mapanga pamoja na mikuki
Bakiri Mawila diwani wa kata ya Lisimonji wilayani humo alidai kuendelea kuwa na hifadhi za vijiji (WMA's) ni kujidanganya Kwa kuwa hifadhi hizo zimevamiwa na wafugaji Kwa kulima ,kuchunga mifugo pamoja na kukata miti Hali inayoondoa hadhi ya uhifadhi huo
Mawila alifafanua kuwa kitendo Cha wafugaji kubaki katika hifadhi huku wakiharibu Mazingira ya uhifadhi ni heri Sasa tupendekeze kuondoa uhifadhi huo Ili maeneo hayo yatumiwe na wananchi katika shughuli za kilimo badala ya kuwaacha wafugaji pekee wakiharibu Mazingira ya hifadhi huku wananchi wengine wakilalamikia kuondolewa katika maeneo hayo kupisha hifadhi.
Salumu Kabumaye Diwani wa kata ya Mchomoro alidai muda wa kupendekeza kufutwa Kwa hifadhi hizo umefika ili kuondoa malalamiko ya wananchi kuwa tunawaoneo wakulima na kuwapendelea wafugaji Kwa kuwaondoa wakulima katika hifadhi na kuwaacha wafugaji katika hifadhi.
Gervas Mwalyombo afisa misitu wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo alisema nguvu za ziada zinahitajika kuwaondoa wafugaji waliovamia katika maeneo ya misitu ya hifadhi lakini Kwa kuwategemea watumishi wa idara ya misitu na wanyamapori pekee hawataweza kwani huhatarisha maisha Yao Kwa kupigwa na mikuki na mishale kutoka Kwa wafugaji hao alisema Mwalyombo.
Mapendekezo ya kufutwa Kwa hifadhi hizo yanatarajiwa kufikishwa katika baraza la madiwani Ili yapitishwe na waheshimiwa madiwani katika kikao Cha baraza la madiwani linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: 2 Barabara ya Boma, S.L.P 55, 57382 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0767519181
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.