WADAU WA MAENDELEO NAMTUMBO WATAKA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI UIMARISHWE.
Na Yeremias Ngerangera...Namtumbo.
Wakiongea kwenye kikao Cha ushauri kupendekeza mpango na bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo wadau wa maendeleo waliwataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani.
Ally Lyuma mkazi wa mamlaka ya mji mdogo wa Namtumbo alisema ipo haja ya uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani Kwa kuwa mfumo huo una manufaa Kwa wakulima wa kipato Cha chini.
Lyuma alifafanua kuwa toka kuanza kutekeleza mfumo huo wa stakabadhi ghalani wakulima wamekuwa na uhakika wa kuuza mazao yao pamoja na kujihakikishia bei nzuri ya mazao yao.
Lukas Sesilius meneja wa chama Cha msingi Naikesi alisema wakulima wa chama Cha msingi Naikesi wanaishukuru serikali Kwa kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani Kwa kuwa wakulima hao wanauhakika na soko la mazao yao Pamoja na bei nzuri.
Kassimu Gunda diwani wa kata ya Likuyu alidai wanaolalamikia mfumo wa stakabadhi ghalani kuwa haufai hao sio wakulima ni wafanyabiashara waliozoea Kununua mazao Kwa wakulima kwa bei ya chini na kwenda kuuza kwa bei ya juu.
Gunda alifafanua kuwa wanaolalamikia mfumo haufai ni wale waliokuwa wanunuzi wa mazao ya wakulima na Kwa kuwa mkulima kwa Sasa anauza mazao yake kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani umewanyima fursa wafanyabiashara Kununua mazao hayo Kwa bei ya chini kutoka Kwa wakulima alisema Gunda.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Juma Pandu aliwasisitizia wataalamu kuimarisha mfumo wa stakabadhi ya ghala Kwa kuwa una manufaa Kwa wakulima wa Namtumbo.
Pandu aliagiza kuwepo na mikakati mizito kudhibiti mapungufu katika kukusanya mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo .
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo pamoja na mambo mengine aliwaahidi wajumbe wa kikao hicho kuwa yeye na wataalamu wake watayafanyia kazi maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa kwenye kikao hicho.
Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya pamoja na kuwashukuru wajumbe kwa michango yao alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri kwa kufunga mfumo wa GOTHOMIS katika Hospitali ya Wilaya Namtumbo ambao unaongeza mapato ya Hospitali hiyo.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: 2 Barabara ya Boma, S.L.P 55, 57382 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0767519181
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.