WANANCHI NAMTUMBO WALALAMIKIA KUCHELEWA UCHIMBAJI MADINI YA URANI.
Wananchi wa mamlaka ya mji mdogo wa Namtumbo Mkoani Ruvuma wamelalamikia kuchelewa kuanza Kwa mradi wa uchimbaji wa madini ya Urani.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara na mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vitta Rashid Kawawa ,walisema tunashangaa kuona mradi wa uchimbaji wa madini ya Urani umebaki kimya licha ya kupewa matumaini ya kuanza Kwa mradi huo.
Shami Kingovaye mwananchi wa kata ya Rwinga mamlaka ya mji mdogo wa Namtumbo alihoji ukimya wa kuanza Kwa uchimbaji wa madini ya Urani katika Kijiji Cha Likuyuseka wilayani Namtumbo.
Kingovaye alidai wananchi wa Namtumbo walikuwa na matumaini makubwa ya kuanza Kwa mradi huo kutawanufaisha wananchi kiuchumi Kwa kuuza bidhaa zao kupitia mkusanyiko wa watu watakaokuwepo wakati wa uchimbaji wa madini huo.
Pia Kingovaye alisema wananchi wa Namtumbo walitegemea kupata ajira mbalimbali kutokana na kuanza Kwa mradi huo lakini wanashangaa ukimya wa kuanza Kwa mradi huo.
Rashid Nihuka Kwa upande wake alihoji Kuna maana Gani ya kuanzisha stendi ya wilaya wakati magari ya vijijini yanapitiliza na kuelekea Songea na wananchi kuendelea kununua bidhaa songea na kuziacha bidhaa za hapa Namtumbo.
Nihuka alihoji wakati wa barabara ya vumbi kabla ya kuwekwa lami nauli ya Namtumbo mpaka Songea ilikuwa shilingi 2500 mpaka 2000 ilikuwa unafika songea lakini baada ya kuwekwa lami nauli zimepanda mpaka 4000 mpaka 3500 alisema Nihuka.
Mbunge wa Namtumbo Vitta Kawawa pamoja na kuwashukuru wananchi wa kata ya Rwinga kutumia muda wao na kuhudhuria mkutano wake Ili waweze kuelezea kero zao.
Kawawa aliwaeleza wananchi wa kata ya Rwinga kuwa haijawahi kutokea katika awamu zote za Marais Namtumbo kupata miradi kama ilivyopata safari hii ya Dkt Samia Suluhu Hassan .
Akijibu kero ya kuchelewa kuchimba madini ya Urani Kawawa alisema Kuna changamoto iliyojitokeza kati ya TANAPA na kampuni iliyopewa jukumu la kuchimba madini hayo.
Kampuni ya Mantra iliyopewa jukumu la kuchimba madini hayo ilikumbana na kikwazo hicho na kusubiria utaratibu mwingine unaofanywa na Serikali alisema mbunge huyo.
Aidha Kawawa alifafanua kuwa awali changamoto ilikuwa eneo linalotakiwa kuchimba madini hayo lipo katika hifadhi na eneo ambalo ni urithi wa Dunia( world heritage) na kulingana na Sheria za kimataifa za uhifadhi hazitakiwa kufanyika shughuli yoyote ya kibinadamu bila idhini ya mamlaka husika.
Kawawa aliwaambia mwananchi kuwa Serikali ililiondoa eneo Hilo kwenye hifadhi Ili kuiwezesha kampuni ya Mantra iliyopewa idhini ya kuchimba madini hayo iweze kuchimba ,hata hivyo kampuni hiyo haikuweza kuanza mradi wa kuchimba madini hayo baada ya kushuka bei katika soko la Dunia.
Wakati kampuni hiyo ikisubiri bei nzuri katika soko la Dunia eneo Hilo la hifadhi ambapo Serikali iliamua kulitoa kwenye hifadhi kutoka hifadhi ya taifa ya selou Kwa wakati ule na kukitenga kipande Cha eneo kilichokuwa na madini ya Urani na kukipa jina la Undendeule forest Ili kuruhusu madini hayo yaweze kuchimbwa Kwa manufaa makubwa ya taifa lakini baada ya hifadhi kuitwa hifadhi ya taifa ya Nyerere na kuwa chini ya TANAPA na Kwa Mujibu wa mbunge alisema imejitokeza changamoto Tena kwa TANAPA kuhusu kutokuwa na taarifa ya uchimbaji huo wa madini katika maeneo ambayo yapo chini Yao lakini Serikali inalifanyia kazi alisema Kawawa.
Kuhusu nauli za mabasi mheshimiwa Kawawa aliwataka wananchi kuwa na subira atalifuatilia jambo Hilo kwenye mamlaka husika na kuhusu stendi ya wilaya alisema atalipeleka kwenye vikao vya kisheria vya maamuzi vya wilaya Ili likajadiliwe na kupatiwa majawabu yake.
Mbunge wa Namtumbo Vita Kawawa anaendelea na ziara yake ya kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara Kwa kusikiliza kero na kuzipatia majawabu Kwa kushirikana na wakuu wa idara wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: 2 Barabara ya Boma, S.L.P 55, 57382 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0767519181
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.