WANANCHI NAMTUMBO WALALAMIKIA UKUBWA WA JIMBO LA NAMTUMBO
.
Wakizungumza kwa masikitiko makubwa kwenye ziara ya Mbunge wa Jimbo hilo Vitta Rashidi Kawawa ,wananchi hao walisema jimbo la Namtumbo ni kubwa sana hali inayomfanya mbunge wao kufanya kazi kubwa ya kuzungukia jimbo hilo na kuwahudumia wananchi .
Ajira ghaibu Kuluchi mwananchi wa kijiji cha Magazini alimwambia mbunge wa jimbo la Namtumbo kuwa Jimbo la Namtumbo ni kubwa mno hali inayomfanya mbunge wao kuzungukia jimbo hilo na kuzungumza na wananchi kwa kutumia muda mrefu ukifananisha na ukubwa wa majimbo mengine.
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Namtumbo Zuberi Lihuwi pamoja na kukiri kuwa Jimbo la Namtumbo ni kubwa alifafanua kuwa vikao vya kisheria vya maendeleo vya wilaya( DCC) pamoja na vikao vya kisheria vya maendeleo vya mkoa vimepitisha maombi hayo ya kuomba jimbo la Namtumbo kugawika na kuwa majimbo mawili.
Hata hivyo Lihuwi alifafanua vigezo vya kugawa jimbo ni kuwa na idadi kubwa ya watu pamoja na ukubwa wa eneo la wilaya yetu hivyo akadai sensa ya mwaka 2022 itasaidia mamlaka kuona malalamiko ya wananchi ya Namtumbo yanaukweli kiasi gani alisema Lihuwi.
Pamoja na Hayo Lihuwi aliwataka wananchi kuwa watulivu kuhusu ujenzi wa barabara ya mtwarapachani –Nalasi mpaka Tunduru kwa kuwa barabara hiyo ipo kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020-2025 baada ya wananchi hao kudai barabara hiyo kuchelewa kujengwa.
Diwani wa kata ya Magazini Grace Kapinga alimpongeza mbunge wa jimbo la Namtumbo kwa ushirikiano wake anaowapatia wananchi wa kata yake kwa kuhakikisha kero ya muda mrefu ya wananchi wa kata ya magazini kuhusu huduma ya afya inatatuliwa kwa kujengwa kituo cha afya na kupatikana kwa vifaa tiba ili kuanzishwa kwa kituo hicho.
Kapinga pamoja na mambo mengine alimwambia mbunge kuwa wananchi wa kata yake wanafuraha sana kuhusu kupatiwa milioni 500 za kujenga kituo cha afya cha magazini pamoja na kupatiwa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 65.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Aaron Hyera alimshukuru Mbunge wa Namtumbo kwa kuipambania wilaya ya Namtumbo ili kuondoa changamoto za huduma za afya zinazowakabili wananchi wa wilaya ya Namtumbo kuhakikisha fedha zinapatikana za ujenzi wa vituo vya afya na zahanati wilayani Namtumbo.
Vitta Rashid Kawawa Mbunge wa jimbo la Namtumbo aliwashukuru wananchi waliofika katika kuhudhuria mkutano wake na kudai kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan inatekeleza mambo kwa vitendo.
Kawawa aliwaambia wananchi kuwa serikali ya awamu ya sita imetoa fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali wilayani Namtumbo haijawahi kutokea kuwepo kwa utekelezaji wa miradi yenye fedha nyingi kama serikali hii inayoongozwa na DKT Samia Suluhu Hassan.
Hata hivyo Kawawa aliwahatarisha wananchi kuwa kuna wapotoshaji wanapita na kuwadanganya wananchi kuwa barabara ya Mtwarapachani –Nalasi mpaka Tunduru fedha zake zimehamishwa na kupelekwa kujenga barabara ya Lumecha-Kitanda mpaka kidatu mkoa wa Morogoro na kuwataka wananchi hao kuachana na wapotoshaji hao.
Aidha Kawawa alifafanua kuwa Serikali imeweka vipaumbele katika ujenzi wa barabara Nchini ,vipaumbele hivyo vinasema barabara zinazounganisha nchi na nchi kipaumbele cha kwanza ,lakini barabara zinazounganisha mkoa na mkoa kipaumbele cha pili na barabara zinazounganisha wilaya ni kipaumbele cha tatu.
Barabara inayosemwa kuwa zimehamishwa hela na kwenda barabara ya Lumecha mpaka kidatu mkoa wa morogoro hiyo ni barabara ya kuunganisha mkoa na mkoa na ya mtwarapachani –Nalasi mpaka Tunduru barabara hiyo ni ya kuunganisha wilaya kwa wilaya na bado haijapatiwa hela na kuwataka wananchi kuwa na subira wakati serikali inatafuta hela ya kujenga barabara hiyo badala ya kupotoshwa alisema Kawawa.
Wilaya ya Namtumbo ina ukubwa wa kilomita za mraba 20,375.1 ni wilaya kubwa kuliko wilaya zingine za mkoa wa Ruvuma ikifuatiwa na wilaya ya Tunduru yenye ukubwa wa kilomita za mraba 18,000 hali inayowafanya wananchi wa wilaya hiyo kuomba jimbo ili kumwezesha mbunge kuwafikia wananchi wa jimbo lake kwa wakati na kuwahudumia.
Mwisho.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Anuani: 2 Barabara ya Boma, S.L.P 55, 57382 NAMTUMBO
Simu ya Mezani: 0252675008
Simu ya Mkononi: 0767519181
Barua Pepe: ded@namtumbodc.go.tz
Hakimiliki©2021Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Haki zote Zimehifadhiwa.